1 Samuel 7

1 aKisha watu wa Kiriath-Yearimu wakaja na kulichukua Sanduku la Bwana. Wakalipeleka katika nyumba ya Abinadabu juu kilimani na kumweka Eleazari mwanawe wakfu kulichunga Sanduku la Bwana.

Samweli Awatiisha Wafilisti Huko Mispa

2 bSanduku la Bwana lilibakia huko Kiriath-Yearimu kwa muda mrefu, yaani jumla ya miaka ishirini, nao watu wa Israeli wakaomboleza na kumtafuta Bwana. 3 cNaye Samweli akawaambia nyumba yote ya Israeli, “Ikiwa mtamrudia Bwana kwa mioyo yenu yote, basi iacheni miungu migeni na Maashtorethi na kujitoa wenyewe kwa Bwana na kumtumikia yeye peke yake, naye atawaokoa ninyi na mkono wa Wafilisti.” 4Hivyo Waisraeli wakaweka mbali Mabaali yao na Maashtorethi, nao wakamtumikia Bwana peke yake.

5 dKisha Samweli akasema, “Wakusanyeni Israeli wote huko Mispa, nami nitawaombea ninyi kwa Bwana.” 6 eWalipokwisha kukutanika huko Mispa, walichota maji na kuyamimina mbele za Bwana. Siku hiyo walifunga na wakaungama, wakisema, “Tumetenda dhambi dhidi ya Bwana.” Naye Samweli alikuwa kiongozi
Kiongozi hapa maana yake mwamuzi.
wa Israeli huko Mispa.

7 gWafilisti waliposikia kwamba Israeli wamekusanyika huko Mispa, watawala wa Wafilisti wakapanda ili kuwashambulia. Waisraeli waliposikia habari hiyo, waliogopa kwa sababu ya Wafilisti. 8 hWakamwambia Samweli, “Usiache kumlilia Bwana, Mungu wetu, kwa ajili yetu, ili apate kutuokoa na mikono ya Wafilisti.” 9 iKisha Samweli akamchukua mwana-kondoo anyonyaye na kumtoa mzima kama sadaka ya kuteketezwa kwa Bwana. Akamlilia Bwana kwa niaba ya Israeli, naye Bwana akamjibu.

10 jSamweli alipokuwa anatoa hiyo dhabihu ya kuteketezwa, Wafilisti wakasogea karibu ili kupigana vita na Israeli. Lakini siku ile Bwana alinguruma kwa ngurumo kubwa dhidi ya Wafilisti na kuwafanya wafadhaike na kutetemeka hivi kwamba walikimbizwa mbele ya Waisraeli. 11Watu wa Israeli wakatoka mbio huko Mispa na kuwafuatia Wafilisti, wakiwachinja njiani hadi mahali chini ya Beth-Kari.

12 kNdipo Samweli akachukua jiwe na kulisimamisha kati ya Mispa na Sheni. Akaliita Ebenezeri,
Ebenezeri maana yake jiwe la usaidizi.
akisema, “Hata sasa Bwana ametusaidia.”
13 mBasi Wafilisti wakashindwa na hawakuvamia nchi ya Israeli tena.

Katika maisha yote ya Samweli, mkono wa Bwana ulikuwa dhidi ya Wafilisti.
14 nMiji kuanzia Ekroni hadi Gathi, ile ambayo Wafilisti walikuwa wameiteka kutoka Israeli, ilirudishwa kwake, naye Israeli akazikomboa nchi jirani mikononi mwa Wafilisti. Kukawepo amani kati ya Israeli na Waamori.

15 oSamweli akaendelea kama mwamuzi juu ya Israeli siku zote za maisha yake. 16 pMwaka hadi mwaka aliendelea kuzunguka kutoka Betheli mpaka Gilgali na Mispa, akiamua Israeli katika sehemu hizo zote. 17 qLakini kila mara alirudi Rama, kulikokuwa nyumbani kwake, huko pia aliwaamua Israeli. Naye huko alimjengea Bwana madhabahu.
Copyright information for SwhKC